SIMBACHAWENE AWATAKA WATANZANIA WANAOISHI NJE YA NCHI KUFUATA TARATIBU ZA KISHERIA
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI
imetoa rai kwa watanzania wote wanaoishi nje ya nchi kuzingatia
taratibu za kisheria zenye lengo la kuwalinda pamoja na kupata hati za
kusafiri Nje ya Nchi.
Akizungumza hayo jijini Dodoma wakati wa
ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya kupinga biashara haramu ya usafirisha
wa binadamu duniani, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene
amesema kuwa hakuna haja ya watanzania kurubuniwa na watu wenye nia
mbaya wanaojitangaza kuwa na uwezo wa kuwatafutia kazi Nje ya Nchi au
ndani ya Nchi bali utaratibu wa serikali ufuatwe.
‘’ Utaratibu
rahisi ni kibali cha mzazi na serikali ya kijiji, anapotoka kuja mjini
tunaweza tukajua na kumlinda katika kuangalia haki zake na kuangalia
endapo atapata madhara yoyote, cha kushangaza watu wanaofanya kazi hiyo
hawataki kufuata taratibu za kisheria ambazo zimewekwa na serikali’’
amesema Waziri Simbachawene.
Waziri Simbachawene amewataka
majirani, wanaposikia manyanyaso katika familia Fulani kwa mtoto ambae
siyo wa familia hiyo ni vema wakatoa taarifa kwenye kituo cha polisi au
uongozi wa mamlaka za serikali.
Pia ameongeza kuwa wapo
watanzania walioenda Nje ya Nchi kama Dubai na kwingineko kwa kufuata
utaratibu uliopo ikiwa ni pamoja na kujaza mikataba ya ajira ambayo
imethibitishwa na ofisi za balozi za Tanzania pamoja na wizara
zinazohusika na ajira hapa Nchini.
‘’Waliowengi wapo salama huko
waliko na hawapati mateso ya aina yoyote kwaiyo ukifuata utaratibu
kimsingi maisha hata huko uliko yanakua salama’’ Amesema Simbachawene.
Aidhaa
Waziri Simbachawene amesema kuwa itifaki ya kimataifa ya mwaka 2000
ilifikiwa na ilikua na madhumuni matatu makuu, ikiwemo kuzuia na kupinga
usafirishaji haramu wa binadamu hususani wanawake na watoto, pili
kuwalinda na kuwatetea wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa
binadamu ikiwa ni pamoja na kuheshimu haki zao pamoja na kukuza na
kuhamasisha ushirikiano miongoni mwa Nchi wanachama ili kufikia malengo
ya kuzuia na kupambana na biashara haramu.
Nae mwakilishi kutoka
shirika la kulinda na kutetea haki za watoto Nchini, SAVE THE CHILDREN
amesema shirika lao limeanzisha miradi maeneo mbalimbali ikiwemo
Zanzibar pamoja na mikoa ya Iringa, Dodoma, Rukwa, Morogoro, Kigoma na
Kasulu lengo likiwa kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi
pamoja na kupinga ukatili wa aina yoyote ile ikiwemo biashara ya
binadamu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya kuzuia na
kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu, Adatus Magere amesema kuwa
kwa mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha siku hiyo mwaka 2019, ambapo
serikali kwa kushirikiana na wadau ilifanya mambo mbalimbali ikiwemo
kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, kutoa ushauri bure wa
kisheria kwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu pamoja na kufanya
kongamano la kitaifa kuhusu biashara haramu ya biandamu.
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya upingaji biashara haramu jijini Dodoma.
Maoni
Chapisha Maoni